Mkristo anaruhusiwa kumwacha mke/mume kwa uzinzi?

uliza ujibiweCategory: Malezi na NdoaMkristo anaruhusiwa kumwacha mke/mume kwa uzinzi?
Merry asked 2 years ago

BWANA YESU ASIFIWE!
NINGEPENDA KUJUA KAMA MKRISTO ANARUHUSIWA KUMUACHA MKEWE AU MUMEWE KWA UZINZI.NIMESOMA mathayo 19:1-9

lakini ninependa kujua zaidi, kwa wanaoijua biblia vyema naomba msaada wenu.
MUNGU AWABARIKI SANA.

1 Answers
Tina answered 2 years ago

Shalom!

Kuhusu swali lako fupi kabisa, lakini linalohitaji ufafanuzi mkubwa, uliloliuliza iwapo Mkristo anaruhusiwa kumwacha mke/mume kwa uasherati, mimi najibu kama ifuatavyo:-
 
Katika ufahamu wangu, na pia kutokana na nilivyojifunza kutoka kwa watumishi mbalimbali, ni kwamba kuna tofauti kati ya UZINZI na UASHERATI kimatumizi.
 
UZINZI ni dhambi inayofanywa na watu waliooana tayari na wanaishi pamoja. Moja anapotoka nje ya ndoa yake na kufanya ngono na mtu asiye mke/mume wake huyo anafanya UZUNZI.
 
UASHERATI ni dhambi inayofanywa na watu ambao hawajaoa au kuolewa bado. Hawa ni pamoja na WACHUMBA wanaotarajia kuoana. Moja kati ya hawa wote anapokuwa anafanya ngono na mtu yeyote, anakuwa anafanya UASHERATI.
 
Maandiko yanasema katika Mathayo 19:9….”Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya UASHERATI, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini. Kutokana na maelezo niliyoyaeleza hapo juu, maandiko haya aliyoyasema Yesu, yanaonesha kuwa wanaozungumziwa kufanya uasherati ni watu ambao ni wachumba kama tulivyozoea kuwaita.
 
Yesu hapa alikuwa akizungumza na jamii mchanganyiko, wengine bila shaka walikuwa na wachumba wao na wengine walikuwa tayari wanaishi pamoja kama mume na mke n.k. Yesu alipokuwa akitaja neno UASHERATI kwa wenzetu wa nyakati hizo, tayari walikuwa wanaelewa kuwa sentensi hiyo ilikuwa inamhusu nani, na kama nilivyokwisha kusema sasa, sentensi hiyo ilikuwa inawahusu wale ambao hawajaanza kuishi pamoja kama mke na mume.
 
Ni kwamba, katika biblia hakuna mahali tunapoweza kupaona pakiwa na neno “mchumba”. Nyakati za biblia watu waliofikia hatua zote za kuoana hata kabla ya kuanza kuishi pamoja, waliitana mke na mume. Ukweli huu tunauona kwa Yusufu aliyemposa Mariamu. Kabla hawajakaribiana Yusufu aligundua kuwa Mariamu alikuwa na mimba. Lakini hapa tunaambiwa kuwa Yusufu alikuwa MUMEWE kama tunavyoweza kuona katika maandiko, [Mathayo 1:18-20 Kuzaliwa kwake Yesu kulikuwa hivi, Mariam mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, MUMEWE, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu KUMWACHA kwa siri. …..malaika wa Bwana alimtokea katika ndondo, akisema Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariam MKEO…..] Hata hivyo inawezekana tatizo hili lilitokana na watafsiri wa maandiko, hawakuweza kuyachukua kama ilivyokusudiwa. Wataalam zaidi wanaweza kutusaidia. Lakini tunachotakiwa hapa kukijua ni kwamba Yesu alikuwa anazungumzia wachumba kwamba wanaweza kuachana.
 
Mariam alikuwa mchumba wa Yusufu lakini maandiko yanataja kuwa mariamu MKE wa Yusufu. Tunajifunza kuwa, kumbe mchumba tunaweza kumwacha iwapo atakuwa amefanya UASHERATI kama tulivyoangalia huko nyuma.
 
Ili kujua kuwa Uasherati na Uzinzi katika maandiko ya biblia zetu za kiswahili ni vitu viwili kiutendaji, tunaweza kuona katika Mathayo 15:19 tunasoma hivi, “Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, UZINZI, UASHERATI; wivu ushuhuda wa uwongo….” andiko hili na mengineyo ya aina hii, yanatuonesha wazi kuwa uzinzi na uasherati ni vitu viwili tofauti katika utekelezaji wake, ndiyo maana yameandikwa yote mawili.
 
Ili kuzidi kufahamu zaidi tofauti ya maneno haya mawili, tunaweza pia kuona yule mwana mpotevu katika kitabu cha Luka, ambaye mali yake aliimalizia kwa uasherati wala si kwa UZINZI kwa sababu alikuwa hajaoa. [Luka 15:13….akasafiri kwenda nchi za mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya UASHERATI].
 
Kimsingi watu waliokwisha kuoana na wanaishi pamoja, maandiko yanakataza kabisa kuwa wasiachane, ndiyo maana maandiko yanasema kuwa tangu mwanzo Mungu hakuruhusu jambo hilo. Musa aliruhusu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao [Mathayo 19:8…..Musa kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi].
 
Mungu anasema anachukia kuachana, na kama anachukia kuachana basi hawezi kuliruhusu jambo la kuachana kwa sababu yoyote ile, [Malaki 2:16 Maana mimi nachukia kuachana, asema Bwana Mungu wa Israel; ….basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiyana]. Maandiko yanazidi kusema wazi juu ya jambo hili katika Luka 16: 18 kuwa “KILA AMWACHAYE MKEWE NA KUMWOA MKE MWINGINE AZINI; NAYE AMWOAYE YEYE ALIYEACHWA NA MUMEWE AZINI” Maagizo haya ya Yesu, Paulo naye kwa kuuona umuhimu wake aliyakumbushia kwa Wakorinto waliokuwa wanaelekea uasi mkubwa ambayo tunayaona katika 1Wakorinto 7:10-11 nayo yanasema “Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi ila Bwana; mke asiachane na mumewe lakini ikiwa ameachana naye, na akae ASIOLEWE, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe”
 
Kuhusu Mathayo 19:9, kwa kifupi tunajifunza kuwa, mke ambaye bado hatujaanza kukaa naye, ambaye sisi wa nyakati hizi tumezoea kumwita “MCHUMBA” pale tutakapogundua kuwa amefanya UASHERATI wakatu wa uchumba tunayo ruhusa ya kumwacha!
 
Ndivyo nijuavyo mimi, hata hivyo sijaweza kuelezea vizuri sana kutokana na kushindwa kupangilia mawazo niliyo nayo juu ya jambo hili. Iwapo kuna mwenye maelezo mazuri zaidi anaweza akafafanua zaidi ili tuzidi kujifunza.
Amani ya Bwana itufunike!

Your Answer