Hazina iliyofichika

Kwanza tambua kwamba Mbinguni ni nchi, na nchi ya Mbinguni ni nchi ya Kifalme, kama vile Tanzania ilivyo nchi ya Kidemokrasia. Unaposoma kwenye Biblia katika kitabu cha Waebrania 11:15-16  maneno ya Mungu yanasema hivi:- “15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16 Lakini badala yake wanatamani nchi iliyo bora zaidi, yaani, nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandalia mji kwa ajili yao” . Kwa hiyo mbinguni ni nchi na utawala wake ni wa kifalme wala siyo demokrasia. Mbinguni ni makao mkuu ya Mungu.

Tunamwamini  Yesu, tunamtumikia  Yesu  na kumfuata Yesu Kristo  ambaye ni Mfalme kwa fikra na mitazamo tuliyojifunza kutoka kwenye jamii , serikali na tamaduni zetu ambazo ziko tofauti kabisa na Ufalme wa Mungu,  ndiyo maana Wakristo  waliozaliwa na kukulia katika nchi za kidemokrasia na dini zenye mapokeo mbali mbali wanapita katika kipindi kigumu sana cha kumtumikia Mungu, kwa sababu wanajaribu kumtumikia Mungu ambaye utawala wake ni wa kifalme kwa mitazamo na fikra za kidemokrasia na dini, wakati demokrasia na ufalme ni vitu viwili tofauti.  Huwezi kuishi katika ufalme wa Mungu na kupata haki zako kwa mitazamo na fikra za kidemokrasia na dini.

Ndiyo maana BWANA Yesu alipoanza kuhubiri alisema hivi :- Tubuni: kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia (Mathayo 4:17). Toba (Repent – change in your mind, change your belief system, change the way you think, to think differently) badili mfumo wa fikra zako, badili mtazamo.

Ujumbe muhimu  sana katika mwili wa Kristo leo ni ujumbe wa Ufalme wa Mungu, ni ujumbe ambao Yesu Kristo mwenyewe alihubiri kila mahali alipokwenda. Yesu Kristo hakuhubiri , baraka wala uponyaji, wala hakuhubiri utoaji wa mapepo wala kufufua wafu, ila alichokihubiri ni Ufalme wa Mungu. Kwasababu ukiwa kwenye Ufalme wa Mungu hayo yote ni kawaida kutokea. Sisi tunayoiita miujiza  ni jambo la  kawaida kutokea ukiwa katika Ufalme wa Mungu ndiyo maana Yesu Kristo mwenyewe hakuhubiri kuhusu miujiza ila alichokihubiri ni Ufalme wa Mungu,  “Lakini Yeye akawaambia, Imenipasa kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.” (Luka  4:43).

Mwanadamu wa kwanza alipewa ufalme na Mungu na alipoasi alipoteza ufalme na kupoteza kila ahadi zilizokuwa ndani ya ufalme. Na kati ya ahadi alizokuwa amepewa mwanadamu ni uhuru wa kula matunda ya kila mti (free access). Kwa hiyo mwanadamu alipomwasi Mungu na kupoteza ufalme, alipoteza uhuru wa kula matunda ya kila mti (free access). Hivyo mwanadamu kuanzia pale akaanza kujitafutia chakula, mavazi, makazi na mambo mengine kama hayo ambayo mwanadamu anahangaika kuyatafuta mpaka leo hii.

Yesu Kristo hakuja duniani kuleta dini ila alileta ufalme, yaani alileta kile ambacho Adam wa kwanza alikipoteza zikiwemo ahadi zote zilizomo ndani ya Ufalme wa Mungu. Ndiyo maana Yesu Kristo alisema hivi:- “Msisumbuke, basi, mkisema, ‘Tule nini?’ Au ‘Tunywe nini?’ Au ‘Tuvae nini?’ Kwa maana hayo yote mataifa huyatafuta; Kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa  mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza Ufalme wake, na haki yake; na haya yote mtazidishiwa.”  Mathayo 6:31-33.

Ufalme wa Mungu unatafutwa, na ukiupata utayaacha yote unayoyahangaikia kila siku. Hebu tazama Yesu alivyokuwa akiuongelea ufalme wa Mungu:-

Yesu anavyoufananisha ufalme wa Mbinguni:-

Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile.

Tena, ufalme wa Mbinguni unafanana na mfanya biashara mmoja mwenye kutafuta lulu nzuri. Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda, akauza yote aliyokuwa nayo, akanunua lulu ile. Mathayo 13:44-46.

Yesu akawaambia mfano mwingine, akasema: ‘‘Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. Mathayo 13:24

Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa Mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua akaipanda shambani mwake. Mathayo 13:31

Akawaambia mfano mwingine, ‘‘Ufalme wa Mbinguni unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika vipimo vitatu vya unga mpaka wote ukaumuka.’’ Mathayo 13:33

“Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama wavu wa kuvulia samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. Mathayo 13:47

Kumbuka dunia hii iko chini ya utawala wa falme mbili tu, Ufalme wa Mungu na ufalme wa shetani. Na kila mwanadamu yuko chini ya utawala mmojawapo inawezekana hujui au unajua. Kumbuka hili “Ufalme wa Mungu unatafutwa bali ufalme washetani hautafutwi”. Kwa hiyo kama haupo kwenye ufalme wa Mungu moja kwa moja upo kwenye ufalme wa shetani.

Utajuaje kwamba upo katika ufalme wa Mungu au wa shetani?
Ukititaka kujua kama upo kwenye ufalme wa Mungu angalia kama una tabia zifuatazo:- upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi na mambo mengine yanayofanana na hayo.

Ukititaka kujua kama upo kwenye ufalme wa Shetani angalia kama una tabia zifuatazo:- Uasherati, uchafu, ufisadi, kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo.

Hiki ni kipimo kizuri cha kujitambua ya kwamba upo katika ufalme wa Mungu au wa shetani.

Kumbuka Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichika shambani.

Mungu akubariki sana

By
Dawson Kabyemela
Kingdom Influence Network.