Jinsi ya kuingia katika Ufalme wa Mbinguni

Mbinguni ni nchi kama nchi zingine, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha  Waebrania 11:15-16  maneno ya Mungu yanasema hivi:- “15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16 Lakini badala yake wanatamani nchi iliyo bora zaidi, yaani, nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandalia mji kwa ajili yao”.

Ili uwe raia wa nchi yoyote ni lazima uzaliwe katika nchi hiyo. Mwanadamu alipomwasi Mungu jambo moja wapo alilopoteza ni uraia wa Mbinguni, kwa hiyo ili upate tena kuwa raia wa Mbinguni ni lazima uzaliwe mara ya pili kwa njia ya Roho mtakatifu, kwa kumpokea Bwana Yesu ili awe Bwana na mwokozi wa maisha yako.

Yesu alikuja duniani akiwa na lengo moja tu la kurudisha kila alichokipoteza mwanadamu, na kubwa ambalo mwanadamu alilipoteza baada ya kutenda dhambi ulikuwa ni Ufalme wa Mungu (Uraia wa Mbinguni). Unaposoma kitabu cha nabii Isaya Mungu anaahidi kurudisha kile ambacho mwanadamu alikipoteza ambacho ni Ufalme,

“Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani hayatakuwa na mwisho kamwe, katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; kuuthibitisha na kuutegemeza kwa hukumu na kwa haki, tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakao tenda hayo. Isaya 9:6-7

Vitu vyote ambavyo mwanadamu alivipoteza baada ya kumwasi Mungu, vilikuwa viko katika mfumo wa Ufalme wa Mungu, kwa hiyo ukiupata Ufalme wa Mungu unakuwa umevipata vyote vilivyopotea baada ya mwanadamu kutenda dhambi, ndiyo maana imeandikwa “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mathayo 6:33.

NB: ukiutafuta ufalme wa Mungu, unakuwa kama sumaku ukivuta vitu vingine vije kwako, (don’t seek things seek the kingdom and other thinks will be added to you, you will attract them).

Mtu mmoja Mfarisayo jina lake Nikodemo mkuu wa Wayahudi huyu alimjia Yesu usiku na kumuuliza habari ya miujiza ambayo Yesu anaifanya, Yesu alimjibu hivi “amin, amin, nakuambia, mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona Ufalme wa Mungu ”. Nikodemo akaendelea kuuliza “mtu awezaje kuzaliwa mara ya pili akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?” Yesu akamjibu hivi:- ‘‘Amin, amin nakuambia, hakuna mtu ye yote anayeweza kuingia katika Ufalme wa Mungu isipokuwa amezaliwa kwa maji na kwa Roho. Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho. Kwa hiyo usishangae ninapokuambia huna budi ‘kuzaliwa mara ya pili’”. Yohana 3:1-7.

CHUKUA HATUA SASA

Inawezekana kabisa ya kuwa wewe unayesoma ujumbe huu hujaingia kwenye Ufalme wa Mungu – yaani hujampokea Yesu Kristo ndani ya moyo wako kuwa Bwana na Mwokozi wako. Lakini sasa umeona umuhimu wa kumpokea Yesu Kristo katika maisha yako.

Mpendwa msomaji, maisha ya mwanadamu yanadai maamuzi kila siku, ili kufanikisha mambo na mipango mbali mbali ya maisha. Uamuzi muhimu wowote mwanadamu anaweza kuufanya ni kumpa moyo Bwana Yesu ili autawale.

Kila mwanadamu anakabiliwa na uamuzi huu muhimu. Hii ni kwa vile tangu mwanadamu wa kwanza Adamu alipoasi katiaka bustani ya Edeni wanadamu wote waliofuata wamerithi asili hii mbaya ya dhambi na uasi. Hata mwanadamu mzuri sana kiasi gani amebeba asili hii ya dhambi (Kwa maana wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu. Warumi 3:23).

Naamini Roho Mtakatifu ameweka fursa hii mikononi mwako kwa mpango maalum wa Mungu ili ufike mahali pa kutubu (kubadili fikra/mtazamo) na kuokolewa kutoka dhambini. Inawezekana kabisa, pia ya kuwa hujawahi kuambiwa juu ya umuhimu wa wewe kumpokea Bwana Yesu. Lakini napenda kukuambia ya kuwa ni mpango wa Mungu uokolewe na kutoka dhambini.

Kwa hiyo kama unataka kuingia katika Ufalme wa Mungu na kupata uraia wa Mbinguni – tafuta mahali palipo na utulivu, na usome kwa sauti sala ifuatayo: (ukiweza unaweza kupiga magoti unapoomba sala hii)

“Ee Mungu wangu ulie Mtakatifu. Ninakuja mbele zako. Mimi ni mwenye dhambi. Naomba unisamehe dhambi zangu zote nilizokukosea katika maisha  yangu. Ninatubu kweli. Naomba damu ya Yesu  Kristo iliyomwagika msalabani kwa ajili yangu initakase sasa katika roho yangu na nafsi yangu na mwili wangu. Nimefungua moyo wangu. Bwana  Yesu Kristo nakukaribisha ndani yangu. Ingia kwa uwezo wa Roho wako – uwe Bwana na Mwokozi wangu kuanzia sasa na siku zote. Ahsante kwa  kunisamehe na kwa kuniokoa. Nimejitoa kwako  nikutumikie katika siku zote za maisha yangu. Shetani hana mamlaka tena juu yangu katika jina  la Yesu Kristo. Amina.

Ikiwa umesoma sala hii kwa kukusudia kabisa na kwa imani, basi wewe umeingia katika Ufalme wa Mungu na dhambi zako zimesamehewa na kusahauliwa na Mungu sawasawa na alivyoandika katika neno lake. Damu ya Yesu iko juu yako sasa.

Mambo muhimu ya kuzingati Baada ya kuingia katika Ufalme wa Mungu

Unapoanza maisha haya mapya ya ufalme wa Mbinguni katika Yesu Kristo nakushauri mambo yafuatayo:

1            Uwe tayari kujifunza njia, kanuni, sheria na utamaduni wa Ufalme wa Mbinguni maana tayari umekuwa Raia wa Mbinguni (Wafilipi 3:20).

2            Kubali kuingia katika Ufalme wa Mungu kama mototo mchanga asiyejua kitu chochote, ambaye yuko tayari kutii maelekezo ya viongozi(Luka 18:17)

3            Pata nafasi ya kumwomba Mungu kila siku ili kudumisha mahusiano yako na Mungu, kwa sababu maombi ni mawasiliano na kadri unavyowasiliana na Mungu ndivyo unavyo dumisha mahusiano yako na Mungu (Luka 18:1)

4            Soma Neno la Mungu (Biblia) kila siku ili Neno hilo liweze kubadili jinsi ya kufikiri kwako na uanze kufikiri kama Mungu anavyofikiri na kuona kama Mungu anavyoona. Pia Neno la Mungu linaongeza imani yako. (wakolosa 3:16)

5            Usiache kukusanyika na kushirikiana na wengine waliompokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wao kama wewe ili uimarike zaidi (Waebrania 10:25)

Bonyeza hapa ili ujue nini kimetokea baada ya kumpokea Bwana Yesu.

By
Dawson Kabyemela,
Kingdom Influence Network.