Kinachotokea unapomkiri Bwana Yesu

Tangu unapoomba sala ile ya kumpokea BWANA YESU awe Bwana na mwokozi wa maisha yako (sala ya toba), kuna mambo mengi yanatokea maishani mwako, ila huwezi ukayaona kwa macho, yote yanafanyika katika ulimwengu wa roho ambayo macho ya kawaida hayawezi kuona. Kwanza historia yako yote ya nyuma inafutwa na unaanza maisha mapya pamoja na Mungu, “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya ” (2korintho 5:17).

Imeandikwa wazi kabisa katika kitabu cha Waefeso 2:19 ya kuwa; “Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu”.

Unapata neema hii ya Mungu, na sasa unakuwa raia wa Mbinguni – biblia inakuambia tangu sasa wewe si mgeni wala mpitaji katika Ufalme wa Mungu – bali wewe ni mwenyeji pamoja na watakatifu wengi waliomo katika nyumba ya Mungu!

Nia ya Roho Mtakatifu kukupa nafasi ya kusoma ukurasa huu, ni kukufahamisha angalau kwa kiasi fulani juu ya umuhimu wa kutubu dhambi zako, na kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako.

Ukisoma ukurasa huu utakusaidia kujua kitu gani kinatokea unapo mpokea Bwana Yesu na mambo muhimu ya kufanya katika maisha hayo mapya ya Ufalme wa Mungu.

Matokeo ya Kumpokea Bwana Yesu

 •      Unasamehewa dhambi zako zote!

“Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu…. Aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani …” (Wakolosai 2:13,14).

“Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote” (1Yohana 1:9).

 •      Unahamishwa toka katika ufalme wa shetani na kuingizwa katika Ufalme wa Mungu.

“Naye alituokoa katika nguvu za giza, na akatuhamisha na kutuingiza katika    Ufalme wa mwana wa pendo lake;” Wakolosai 1:13.

Kuna falme mbili zinazopingana na kila mtu ni raia katika mojawapo wa falme hizi. Kuokoka ni kuondolewa katika ufalme wa giza (shetani) na kuhamishiwa katika Ufalme wa Mungu. Unakubali  kutubu na kumwelekea Mungu si tu unasamehewa dhambi lakini pia unahamishwa na kuingizwa katika Ufalme wa Bwana Yesu (mwana wa pendo la Mungu) ukiwa katika Ufalme wa Mungu huna haja tena na msaada wa shetani katika maisha yako. Hirizi, utabiri wa nyota, mazindiko, ibada za mizimu na ibada za kimila huvihitaji tena. Ulipotubu umebadili msimamo na mwelekeo wako hivyo unaviondoa vitu hivi katika maisha yako maana wewe si raia wa ufalme wa shetani hata kautii na kuutumikia. Yesu ndiye mfalme wako na anawajibika kukulinda.

 •     Jina lako linaandikwa mbinguni!

“…furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni” (Luka 10:20).

“Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake” (Ufunuo 3:5).

 •      Unakuwa mwanfunzi wa Yesu.

“Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho mtakatifu.” Mathayo 28:19

 •      Unakuwa kiumbe kipya!

“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya” (2Wakorintho 5:17).

“Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulubiwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiri, bali kiumbe kipya” (Wagalatia 6:14,15).

“Mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu, mkavae utu mpya ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli” (Waefeso 4:22-24).

 •      Umekuwa mtoto wa Mungu!

“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu (Yohana 1:12,13).

“Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo… Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo” (1Yohana 1:1,2).

 •       Malaika wanakuzunguka hata kama huwaoni!

“Je! hao wote (malaika) si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale watakaorithi wokovu? (Waebrania 1:14).

“Kwa kuwa atakuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe” (Zaburi 91:11,12)

 •      Unakuwa makao ya Kristo na Mungu!

“Yesu akajibu, akamwambia, mtu akinipenda atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake” (Yohana 14:23)

“Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu” (Wagalatia 2:20).

“Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho” (Waefeso 2:22).

 •      Roho Mtakatifu yumo ndani yako sasa!

“Lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa roho wake anayekaa ndani yenu” (Warumi 8:11).

“Au hamjui ya kuwa miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? (1Wakorintho 6:19).

 •      Una mamlaka juu ya shetani na kazi zake tangu sasa!

“Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru” (Luka 10:19)

“Na ishara hii zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo …. Wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya” (Marko 16:17,18).

“Basi mtiini Mungu. Mpingeni shetani, naye atawakimbia” (Yakobo 4:7).

 •      Utafufuliwa au kunyakuliwa Yesu akija kulichukua kanisa maana unao uzima wa milele!

“Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima” (1Yohana 5:12).

“Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele” (1Wathesalonike 4:16,17).

“Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu …. (Ufunuo 20:6

 • Unahesabiwa haki na Mungu.

Kuhesabiwa haki maana yake ni kuonekana kuwa huna hatia mbele za Mungu. Huna kesi, hivyo una kibali mbele zake.

“kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, wanahesabiwa haki bure kwa neema Yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu. Yeye ambaye Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kwa njia ya imani katika damu Yake. Alifanya hivi ili kuonyesha haki Yake, kwa sababu kwa ustahimili Wake aliziachilia zile dhambi zilizotangulia kufanywa. Alifanya hivyo ili kuonyesha haki Yake wakati huu, ili Yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.” Warumi 3:23-26.

Haya ni baadhi tu ya maneno mengi mazuri ambayo yamo katika biblia yanayoeleza kilichotokea ulipookoka. Nakupa ushauri ya kuwa uyasome mara kwa mara pamoja na mengine yaliyomo katika biblia ili upate kujijua wewe sasa ni nani mbele za Mungu na   za shetani baada ya kuokoka.

By
Dawson Kabyemela,
Kingdom Influence Network.