KUHARIBU VITI VYA ENZI VYA KISHETANI

Kuna viti vya enzi ambavyo vinatumika kufanya uharibifu kwenye maisha ya watu, unaweza kumwangalia mtu ambaye ni mheshimiwa au baba, mama, mjomba au kitu chochote kiko mahali kumbe kinatumika kama kiti cha enzi cha shetani. Ukitaka kufanikiwa lazima ushughulikie viti vya enzi na kama hujashughulika na viti vya enzi huwezi ukafanikiwa, mahali panapoitwa enzi maana yake ni makao makuu ya mtawala fulani. Nchi kama Tanzania ina Raisi ambaye ana makao yake makuu yanayoitwa Ikulu. Ikulu ni jina la Kisukuma ambalo mwalimu nyerere alilipenda akaamua kulitumia. Marekani nayo ina rais wake mwenye kiti chake cha enzi kinachoitwa White House mahala ambapo chemchemi ya umarekani inatokea ni mahala ampaboni kisima cha uchumi na jeshi vinaanzia. Ukienda South Korea utakuta Blue house, ukienda China utakuta Dragon House. ‘Kilivyo kiti cha enzi ndivyo jinsi nchi ilivyo’.

Ni mahali ambapo maelekezo ya kijeshi, kiuchumi yanatokea.

Ukitaka kuikamata nchi huwezi kwenda kuwakamata watu kwenye nyumba zao bali kikamate kiti cha enzi cha nchi hiyo na hapo ndipo utakapoweza kuishika nchi. Nchi zote duniani zinaongozwa kutoka kwenye kiti cha enzi mahali ambapo hata njaa haiwezi kutokea ni mahala penye ulinzi wa kutosha sababu ni kwenye kiti cha enzi.
Shetani naye amejenga viti vya enzi kwenye maeneo mbalimbali kwenye maisha ya watu. Kwasababu watu wengine kupona kwao sio mpaka waombewe bali mpaka kuvipindua viti vya enzi vilivyowashikilia. Kuna viti vya enzi vya kishetani ambavyo vipo ndani ya watu na kuna viti vya enzi ambavyo ni miti mikubwa watu wanaiogopa, pia kuna sanamu watu wanaziinamia ni viti vya enzi vya shetani sababu anapenda kuabudiwa na watu hawa hawawezi kuviacha kirahisi maana yake mpaka uvipindue na kuviteketeza ndipo wataacha kabisa, kuna viti vya enzi vinavyoshikilia familia, kwenye ndoa, kwenye biashara ambavyo ukivipindua utakuwa umeuangusha utawala wote wa aliyekutesa kwenye maisha yako kwa mamlaka ya jina la Yesu. Kila mtu au familia ina kiti cha enzi cha enzi kinachoongoza maisha yao ukikitambua na kukipindua ukakisambaratisha kwa Jina la Yesu kristo utakuwa umeshinda vita kuu asilimia miamoja.

Kwenye Ukristo kiti cha enzi ni madhabahu, ni mahala ambapo Mungu anashuka anasaidia watu , ni mahala ambapo Mungu anashuka anaongea na watu, ni mahala ambapo Mungu anashuka anafungua watu na kuwafundisha wapate maarifa. Shetani naye amejenga viti vya enzi ili kuongoza maeneo fulani au ofisi fulani au kijiji fulani au nchi fulani ukifanikiwa kupiga viti hivyo uwezo wake wa kutawala maeneo hayo unakuwa imekwisha kwa jina la Yesu.

Ufunuo 2: 13 “Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani.”

Andiko hili limeandikwa na Yohana kwenye kisiwa cha Patimo kipo hata leo. Linatuonyesha kuwa kuna mahala shetani anakaa, kwenye ndoa anaweza kuchagua kukaa sehemu fulani akaamua kumruhusu mtu au familia fulani ifanikiwe kwenye maeneo mengine yote isipokuwa sehemu fulani anaamua kukaa pale kuzuia wasipenye. Hapo akaapo shetani huwa ni sehemu ya kukumbwa na kuharibikiwa na misukosuko sana.

1Wafalme 10: 9 “Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa Bwana amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki.”

Matendo 12:

Siku moja herode alitoa hotuba watu wakasifia na kumshangilia wakisema ni Mungu ameongea nao lakini Mungu aliamua kumpiga kwa ugonjwa akafa sababu alikuwa sio yeye bali ni kiti cha enzi ndicho kilichomfanya aongee vile.

Isaya 66: 1 “Bwana asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani? Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.”

Vitu vyote vimewekwa chini ya nyayo zetu na sisi ndio miguu ya kanisa, kwenye kiti cha enzi cha Mungu.

1 Wafalme 22:19 “Mikaya akasema, Sikia basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto.”

Watu ambao wamejengewa viti vya enzi ukiwaombea huwezi kuwasaidia mpaka umfundishe jinsi ya kushindana kwa vita ya kiroho kwa mamlaka ya jina la Yesu kristo,

kuna watu ambao wanacharge kupitia watu ambao ndani yao kuna viti vya enzi vya shetani. Kuna watu wanapenda kukaa baharini wanasema wanapumzika lakini watu wale wengi wao huwa wanacharge rohoni kama viti cha enzi. Shetani ameweka viti vyake vya enzi ndani ya watu.

Ufunuo wa Yohana 12: 4 “Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake.Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi.”

Kwa kawaifa shetani huwa hatafuti watu waliokwisha zaa bali huwa anatafuta walio karibu kuzaa ili azaapo aibe na kuharibu inaweza ikawa ni biashara, ndoa, kazi, n.k Pale unapokaribia kuzaliwa unakuta anawahi aharibu na kuiba. Maana ya mwanamke ni alama ya kanisa na hapa tunaona shetani amejiandaa kukaribia ili amle motto atakayezaliwa lakini ameshindwa kabisa katika jina la Yesu. Tumeona kwenye makusanyiko makubwa ya maji yasiyokauka(baharini) ndipo ameweka kiti chake cha enzi.

Ufunuo 13: 1 “Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru. Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.”

Kuna viti vya enzi ambvyo vipo katika anga, nchi. Ndani ya anga shetani ameweka viti vya enzi.

Huyu ni mnyama aliyetokea baharibi ambaye amepewa enzi ya utawala. Kwa maana hiyo ndiomaana unaskia kuna chunusi kwenye maji, unaskia matukio mengi ya kwenye maji sababu kuna mkuu wake mwenye kiti cha enzi. Kwenye bahari kuna ulimwengu ambao watu wanachukuliwa wanawekwa huko wakimtumikia shetani.

Mithali 24: 11 “Uwaokoe wanaochukuliwa ili wauawe; Nao walio tayari kuchinjwa uwaopoe.”

Nyakati hizi Mungu anawaokoa kwa damu ya mwanakondoo wale wote walioonewa na viti vya enzi vya shetani.

Waefeso 2:2 “ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi”

Mahali penye kiti cha enzi uharibifu unaimarishwa. Mfano ukitaka kuanza biashara au kazi mahali fulani lazima uharibu kiti cha enzi cha mahali hapo unapotaka kufanya bihashara ndipo ufanikiwe. Watu watumishi wa shetani (wachawi, waganga,wasoma nyota, wasihiri n.k) wanaweza kujenga kiti cha enzi ndani ya mtu bila yeye kujijua wakawa wanapata nguvu na kuongoza mambo yao kupitia kwake.

Unaweza kwenda mahali ukaambiwa hapa huwezi kufanya jambo fulani bila kuonana na mtu fulani fahamu huyo ni kiti cha enzi cha kishetani anayetawala eneo hilo. Maanake yeyeya anakuwa ndiye amebeba kiti cha enzi ndani yake kwa kujua au bila yeye kujua na wachawi wakimwona wanakuwa wanaongeza nguvu zao kupitia yeye, anakuwa ndiye madhabahu yao.

Ezekieli 28

Wachawi wanawachukua watu hapa duniani na kwenda kuwauza kuzimu huku huku duniani mwili ukiwa ni kivuli ndani yake kuna pepo au jini.

Unapomkuta mtu anamatatizo anaombewa lakini haponi anatabia mbaya za ajabu na haeleweki fahamu maanayake ndani yake kuna shetani ndilo linaufanya mwili wake uishi sababu mwili bila roho hauwezi kitu.viti vya enzi vipo kila mahali duniani. Watu wengi hawapo ndani ya miili yao na kilichopo ndani yao ni kiti cha enzi cha kishetani. Shetani anaweza kuweka kiti cha enzi mahali popote ili ajenge utawala wake.

Kiti cha enzi kinaweza kuwa kwenye ukoo lakini kinaweza kuwe kwa kiti ndani ya mtu kuumiliki ukoo ili uwe na magonjwa ya kurithi, umaskini , uharibifu, talaka au kuoa/olewa na kuachika. Mtu mwenye kiti cha enzi ndani yake anaweza akawa anajijua au hajijui. Unaweza kukuta mtu anakuwa anamamlaka kwenye ukoo ambaye akisema jambo lazima asikilizwe na linakubalika hata kama ni la ajabu na mara nyingi watu wa namna hii akikuangalia au akikukemea lazima ushtuke uogope hata kama hujatenda kosa maana yake anakuwa yeye ndiye ameshikilia ukoo wote unakuwa wanamwogopa na kumtii yeye kumbe ni kiti cha enzi kilichopo ndani yake ndicho wanakitii, ukikipiga kile kwa jina la Yesu, kinaondoka na mambo ya ajabu kwenye ukoo yanakwisha kabisa.
Ukikiangusha kiti cha enzi basi mahali fulani patafunguliwa na kua huru, iwe ni biashara, ndoa, safari kazi, afya.

“ukiri”
“Kwa mamlaka ya jina la Yesu naangusha viti vyaa enzi kwenye familia yangu kwa jina la Yesu, ninapiga viti vyote vya enzi vinavyoongoza familia na ukoo wangu kwa damu ya Yesu”

Ukikipiga kiti cha enzi kwenye mtaa wako basi mtaa utakombolewa.

Matendo ya mitume 13: 6 “Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu; mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.”

Mtume Paulo alikuwa anamhubiria mkuu wa mkoa ambaye alikuwa anamchawi wake baar yesu ambaye alijaribu kumzuia kichawi Paulo asimhubirie habari njema liwali Yule lakini hakuweza matokeo yake Paulo akamlaani akawa kipofu. Mtu kama bar yesu alikua ni kiti cha enzi kwaajili ya kumshauri na kumwongoza yule liwali. Tunajifunza kumbe viongozi wengi wana waganga wao wa kienyeji ambao ni viti vya enzi vya shetani vinavyowaongoza kufanya maamuzi juu ya watu wanaowatawala.

Paulo alikipindua kiti cha enzi kilichokuwa ndani ya msichana ambaye wafanya biashara na wafanya kazi walikuwa wanakitumia kama kiti cha enzi na baada ya kupigwa mji ulikombolewa ukawa huru jambo lililosababisha akina Paulo wakaenda gerezani.

Matendo ya mitume16:16 “Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu. Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu.

Akamtoka saa ile ile. Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji; wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi; tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi.”

Duniani namna pekee ya kufankiwa lazima uharibu chanzo cha tatizo. Ukiona hufanikiwi maana yake lipo linalozuia, ambalo ukilifahamu na kuliharibu utafanikiwa na kusonga mbele.

Waefeso 6: 12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”

Mashetani sio raia bali ni majeshi ya pepo wabaya waliofundishwa waliokwenda kozi wakasoma wakafuzu hawawezi kufanana na raia kwahiyo ukitaka kuwashinda lazima uwe vizuri rohoni uwapige kwa jina la Yesu utawashinda kabisa. Kwenye kila familia kuna anayeongoza kama kiti cha enzi cha kishetani ukimpiga huyo unaikomboa familia na magonjwa, tabia, umaskini, kuachika na mabaya yote yataondoka kwa mamlaka ya Jina la Yesu kristo. Amen

BY

ASKOFU MKUU DR JOSEPHAT GWAJIMA

UFUFUO NA UZIMA