Kwa nini unahitaji Eden

Msiba mkubwa alionao mwanadamu siyo kifo, bali msiba mkubwa alionao mwanadamu ni kuishi bila kusudi, msiba mkubwa alionao mwanadamu ni kuishi bila kujua kwa nini anaishi, huu ni msiba mkubwa sana kwa kila mwanadamu anayeishi bila kujua ni kwa nini anaishi.

Kwa sababu hakuna kiumbe chochote kilichoumbwa na Mungu bila ya kuwa na kusudi, Neno la Mungu liko wazi kabisa katika kitabu cha Waefeso 1:11 neno la Mungu linasema hivi “Katika Kristo sisi nasi tumepata urithi, tukiisha kuchaguliwa sawasawa na kusudi la Mungu, Yeye ambaye hufanya mambo yote kulingana na mapenzi Yake.” 

Mungu anamlisha na kumtunza mtu kwa kadri anavyotimiza kusudi lake hapa duniani. Yesu alisema hivi:- Mathayo 6:26 “Waangalieni ndege wa angani, wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege?”.

Mungu anawalisha ndege wa angani kwa sababu wanatimiza kusudi la Mungu hapa duniani, huwezi kumkuta hata siku moja ndege wa angani anajaribu kuiga tabia za samaki wa baharini, kwa sababu hilo siyo kusudi la kuumbwa kwake. Wanadamu wanakosa huduma nzuri za Mungu ni kwa sababu hawako kwenye kusudi la Mungu, na Mungu hawezi kukulisha na kukutunza kama huko nje ya kusudi lake.

Note: “The most important discovery in your life is the discovery of your purpose”.

Halikuwa kusudi la Mungu kumuumba na kumweka mwanadamu duniani ili aishi maisha ya mahangaiko na mapambano akitafuta chakula, makazi, mavazi, maradhi, fedha, kazi na mambo mengine yanayofanana na hayo ambayo mwanadamu anahangaika kuyatafuta kila siku, bali Mungu alimuumba mwanadamu kwa mfano wake na kwa sura yake na kumuweka katika bustani ya Eden na kumkabidhi mamlaka- ufalme (Dominion-kingdom) ili mwanadamu aitawale dunia kwa niaba ya Mungu (Mwanzo 1:26).

Kumbuka ya kwamba Eden ni mazingira yenye uwepo wa Mungu (uso wa Mungu), ambapo mwanadamu anakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na Mungu. Hivyo mwanadamu aliumbwa ili aishi Eden yaani katika mazingira yenye uwepo wa Mungu (uso wa Mungu) katika mda na wakati wote awapo duniani.

Mungu alikuwa akitengeneza mazingira/nafasi kwanza ndipo anaumba kiumbe au kitu kitakachokuwa katika mazingira yale.

Sasa nisikilize kwa makini sana ili upate kufahamu na kugundua mahangaiko na matatizo ya mwanadamu yanapoanzia.

Mungu aliumba ardhi halafu akaumba mimea na kuiweka ardhini,

Mungu aliumba mbingu  halafu akaumba nyota na kuziweka katika mbingu,

Mungu aliumba maji halafu akaumba samaki na kuwaweka katika maji,

Mungu aliumba Eden halafu akamweka mwanadamu.

Kwa hiyo basi, mmea uliumbwa ili uishi kwenye ardhi ndiyo mazingira yake, ukiuondoa mmea ardhini hakuna haja ya kuuambia nyauka, utanyauka wenyewe maana umeondolewa kwenye mazingira yake.

Samaki aliumbwa ili aishi majini ndiyo mazingira yake, ukimuondoa samaki majini huna haja ya kumwambia kufa, atakufa mwenyewe ni kwasababu umemwondoa kwenye mazingira yake.

Mwanadamu aliumbwa ili aishi katika bustani ya Eden / mazingira yenye uwepo wa Mungu ndiyo mazingira yake, ukimwondoa mwanadamu katika bustani ya Edeni huna haja ya kumwambia kufa, atahangaika kama samaki ahangaikavyo pindi atolewapo majini na kufa. Watu wengi sana wanaishi maisha ya mahangaiko ni kwa sababu hawapo Eden ( mazingira yenye uwepo wa Mungu / uso wa Mungu ).

Kwa hiyo basi, mimea inahitaji ardhi ili iweze kuishi, nyota zinaitaji mbingu ili ziweze kuishi, samaki wanahitaji maji ili waweze kuishi na wanadamu wanahitaji Eden ili waweze kuishi.

Katika viumbe vyote vilivyoumbwa na Mungu hakuna kiumbe kingine chochote kilichopewa maagizo na Mungu tofauti na Mwanadamu (“BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu. Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula , walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika”. Mwanzo 2:16-17 ).

Kufa siyo pale mtu anapokufa na kuzikwa, kufa ni pale mtu anapotenda kinyume na maagizo ya Mungu, kama Mungu alisema usiibe au usizini au usiue unapofanya hayo unakufa yaani unatengwa na uso wa Mungu.

Maana ya neno kufa ni kutengwa na uso wa Mungu/mkato wa mawasiliano na mahusiano na Mungu / kuondolewa katika uwepo wa Mungu (Eden).

Kumbuka kukaa kwako Eden(uwepo wa Mungu /uso wa Mungu) ndiyo usalama wako, na shetani hawezi kukugusa ukiwa katika uwepo wa Mungu(Eden) na dhambi ndiyo inayotuondoa katika uwepo wa Mungu(Eden).

Kusudi la Mungu kumuumba Mwanadamu

Kumbuka kipindi ambapo mwanadamu alipokuwa akiwekwa katika bustani ya Eden tayari alikuwa amekabidhiwa ufalme/mamlaka (Mwanzo 1:26), kwa hiyo mwanadamu aliingia Eden akiwa na mamlaka ya kutawala vitu vyote alivyo vifanya Mungu (Waebrania 2:6-8).

Ufalme ni program ambayo Mungu aliitengeneza na kuiweka ndani ya mwanadamu ili Mungu aweze kutumia fikra(Mind) za mwanadamu na kutimiza mapenzi yake duniani. Ndiyo maana Yesu alipoulizwa na Mafalisayo ufalme wa Mungu utakuja lini, Yesu alisema hivi “ufalme wa Mungu umo ndani yenu” (Luka 17:20 – 21)

Ufalme ni kama operating system ndani ya kompyuta ambayo Mungu aliiweka ndani ya mwanadamu na anaitumia ili kutimiza mapenzi yake hapa duniani yeye akiwa mbinguni, kumbuka ya kwamba na shetani naye anatumia fikra(Mind) za mwanadamu kutimiza mapenzi ya ufalme wake duniani, Ndiyo maana BWANA Yesu alipoanza kuhubiri alisema hivi :- Tubuni: kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia,

Toba (Repent – change in your mind – change your operating system, change your belief system, change the way you think, to think differently) badili mfumo wa fikra zako.

Mungu anapotaka kutimiza mapenzi yake hapa duniani ni lazima atumie fikra za mwanadamu, na shetani hivyo hivyo.

Mapenzi ya Mungu yanatimizwa kupitia mfumo wa ufalme wa Mungu unapokuja katika fikra zetu, ndiyo maana wanafunzi wa Yesu walipo muuliza jinsi ya kusali alisema hivi:- Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye Mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbunguni (Mathayo 6:9 – 10)

Dhambi inapoingia katika maisha ya mwanadamu inasababisha program ya Mungu inayoitwa ufalme iharibike(corrupt)- kutoka 32:7.

Dhambi ni kirusi kinachoingia katika maisha ya mwanadamu na kuharibu program za Mungu zilizomo katika fikra za mwanadamu.

Damu ya Yesu ni software (antvirus) inayosafisha dhambi (virus) ndani ya mwili wa mwanadamu ili Roho mtakatifu aishi ndani ya mwanadamu huyo.

Kitendo cha mwanadamu kuasi maagizo ya Mungu alipoteza mamlaka (ufalme) ya Mungu duniani na kumkabidhi shetani (Luka 4:6), hivyo mwanadamu akafukuzwa katika bustani ya Eden na mahangaiko ya mwanadamu yakaanzia pale, mwanadamu akaanza kutapatapa kama samaki atapatapavyo pindi aondolewapo majini mpaka sasa bado mwanadamu anatapatapa, mwanadamu bado ananyauka kama mmea uliong’olewa kwenye ardhi, mwanadamu mpaka sasa hajui alipoteza nini na anahangaikia nini. Kwa sababu huwezi kutumia mamlaka/ufalme uliopewa na Mungu nje ya Eden.

Kila mwanadamu anahitaji kuishi Eden kama vile samaki anavyo hitaji kuishi majini kwa sababu ndiyo mazingira yake, ili mwanadamu apate utulivu, amani, furaha ya kudumu anahitaji Eden tofauti na hapo mwanadamu ataishi maisha ya wasiwasi na mahangaiko mpaka kufa kwake

NOTE: You are not created to live without your creater (GOD), otherwise you will struggle to live.

Kwa hiyo baada ya mwanadamu kufukuzwa katika Bustani ya Eden akawa balozi bila hati, mwanadamu akawa mjumbe bila hadhi ya kiofisi, mwanadamu akawa raia bila nchi, mwanadamu akawa mfalme bila ufalme, mwanadamu akawa mtawala bila miliki, mwanadamu akawa mtoto bila Baba, mwanadamu akawa mkimbizi duniani.

By
Dawson Kabyemela,
Kingdom Influence Network.