Mafundisho ya Ufalme

Kama kuna elimu muhimu sana ambayo kila mwanadamu anapaswa kujifunza tangu utotoni, basi ni elimu ya ufalme wa Mungu, kwa sababu kipaumbele cha kwanza cha Mungu kwa kila mwanadamu ni kuutafuta kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake kabla ya jambo lolote ( Mathayo 6:33). Hivyo Mungu anataka kila mwanadamu ajifunze na kuuelewa Ufalme wa Mungu kwanza kabla ya jambo lolote.

Na vita kuu ya shetani aliyonayo kwa mwanadamu ni kwamba hataki mwanadamu aelewe ni nini maana ya ufalme (Mathayo 13:19), shetani hataki mwanadamu ajue Yesu alileta nini duniani.

Mwanadamu amekuwa ni kiumbe pekee aliyeumbwa na Mungu ambaye mwanadamu huyo anaishi maisha magumu, ya  kuangaika na kutapatapa hapa duniani kwa sababu ya kukosa maarifa ya ufalme wa Mungu.

Tumezaliwa na kukulia katika nchi za kidemokrasia, kwa hiyo imekuwa ni vigumu sana kuelewa na kufuata kanuni na taratibu za Ufalme wa Mungu ambazo zenyewe ziko tofauti kabisa na za kidemokrasia, jambo ambalo limewafanya watu wengi sana wanaomtumikia Mungu wanaona maisha ya utumishi ni magumu sana na wengine hata kuamua kuacha kumtumikia Mungu kabisa.

Hii ni kwa sababu wengi wanaingia kwenye Ufalme wa Mungu wakiwa na fikra za  ki-demokrasia pamoja na mapokeo ya kidini, wakati ufalme wa Mungu sio dini wala utawala wake siyo wa ki-demokrasia. Ufalme wa Mbinguni ni nchi na ni nchi yenye utawala wa kifalme kama vile Tanzania ilivyo nchi yenye utawala wa ki-demokrasia, unaposoma kwenye Biblia katika kitabu cha Waebrania 11:15-16  maneno ya Mungu yanasema hivi:- “15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16 Lakini badala yake wanatamani nchi iliyo bora zaidi, yaani, nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandalia mji kwa ajili yao”. Kwa hiyo mbinguni ni nchi na utawala wake ni wa kifalme wala siyo wa kidemokrasia. Mbinguni ni makao mkuu ya Mungu.

Unapoingia katika Ufalme wa Mungu jambo la kwanza ambalo Mungu anaanza kushughulika nalo kwako ni kubadili jinsi ya kufikiri kwako, kwa sababu hakuna chochote kile kinachoweza kubadika ndani ya maisha mwanadamu mpaka amebadili jinsi ya kufikiri kwake (nothing can change in your life until you change in your mind ). Ndiyo maana BWANA Yesu alipoanza kuhubiri alisema hivi :- Tubuni: kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia (Mathayo 4:17). Toba (Repent – change in your mind, change your belief system, change the way you think, to think differently) badili mfumo wa fikra zako, badili mtazamo. Kwa sababu huwezi kuingia katika Ufalme wa Mungu na fikra za kidemokrasia, mapokeo ya kidini au mapokeo ya kimila halafu ukategemea mafanikio ya Ufalme wa Mungu.

Yesu alisema hivi:- “Nami nitakupa wewe funguo (Laws, principles) za Ufalme wa Mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa Mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa Mbinguni” Mathayo 16:19. Funguo za kuingia na kutoka kwenye umaskini, magonjwa, utasa na matatizo mengine kama hayo unazo wewe, tatizo ni kwamba huzijui na hujui jinsi ya kuzitumia. Kingdom Influence Network itakufundisha aina za funguo na jinsi ya kutumia hizi funguo (Laws and principles) za ufalme wa Mbinguni.

Mafundisho mengine ya ufalme wa Mungu.