Mjue adui yako

Adui yetu mkuu siyo shetani wala siyo dhambi, ila ni ujinga. Ujinga ni kutokujua, Ujinga ni ukosefu wa maarifa. Mungu anasema hivi “watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa“(Hosea 4:6), Mungu hakusema watu wangu wanaangamizwa na shetani, bali alisema kinachowaangamiza watu wangu ni ukosefu wa maarifa (kutokujua).

Adui wa kwanza anaye haribu ndoa za watu, biashara za watu, huduma za watu, serikali zetu na maendeleo ya watu, sio shetani bali ni ujinga, na shetani anatumia ujinga ulio nao ili kukutawala. Shetani anapogundua ya kwamba katika eneo fulani wewe ni mjinga, anatumia eneo hilo kukutawala. Kwa hiyo ujinga ni mlango ambao mwanadamu anamfungulia shetani ili amtawale. Eneo ambalo shetani anajua unaufahamu wa kutosha shetani hawezi kuligusa.

Kwa kiebrania neno ujinga(ignorance) limetafsiriwa kama giza(darkness) , ndio maana shetani anaitwa mfalme wa giza(the prince of darkness), maana yake shetani anawatawala watu kwa ujinga walionao, na Yesu pia anawatawala watu kulingana na maarifa waliyonayo. Yesu anajulikana kama nuru ya ulimwengu (Yohana 8:12), kwa Kiebrania neno Nuru(light) limetafsiriwa kama maarifa(Knowledge), Biblia inatuita sisi kuwa ni nuru(maarifa) ya ulimwengu(Mathayo 5:14), maana yake Mungu anataka atumie maarifa tuliyonayo ili kuutawala ulimwengu.

Mungu anatumia maarifa ya watu ili kuwatawala katika ufalme wake, na shetani pia anatumia ujinga wa watu ili kuwatawala katika ufalme wake, na popote palipo na ukosefu wa maarifa(nuru), kuna giza(ujinga) na popote palipo na giza(ujinga) shetani anatawala, kuanzia kwenye familia, jamii, kabila, taifa na maeneo mengine kama hayo. Ndiyo maana Mungu alikununua kwa gharama kubwa sana ili akufanye kuwa nuru(maarifa) na akakuweka katika eneo ulilopo ili shetani asiendelee kutawala mahali hapo kwa ujinga wake.

Nataka nikupongeze kwa hatua ya ujasiri na umakini uliyochukua kwa kusoma ukurasa huu na napenda nikuhakikishie kuwa hutajutia mda wako. Kumbuka maneno ya busara yasemayo:- kama unafikiri elimu ni ghali basi jaribu ujinga “if you think education is expensive try ignorance”.

Lengo kuu la shetani ni kuendelea kupofusha fikra za wanadamu na kuwafanya kuwa wajinga, ili aendelee kuwatawala kwa ujinga wake. 2Korintho 4:4 “ambao ndani yao, mungu wa dunia hii amepofusha fikra zao wasioamini, isiwazukie nuru(maarifa) ya Injili ya utukufu wake Kristo, aliye sura ya Mungu”. Na kati ya mambo ambayo shetani hataki mwanadamu aelewe ni ufalme wa Mungu.

By
Dawson Kabyemela,
Kingdom Influence Network.