Sera ya ufalme wa Mbinguni, kuhusu ujenzi wa nyumba ya kuishi kwa “Raia” wake walioko duniani.

Na  Mwalimu  Christopher & Diana Mwakasege(Mana Ministry)nyumba23

Bwana Yesu asifiwe sana sana!

Je, una nyumba ya kuishi iliyo mali yako, na unaishi ndani yake? Je, una mpango wa kujenga nyumba yako ya kuishi?Je, unajua biblia inasema nini juu ya sera ya ufalme wa mbinguni kuhusu ujenzi wa nyumba ya kuishi kwa “raia” wake walioko duniani?

Mtu anapohitaji ushauri wa kiimani, juu ya ujenzi wa nyumba yake ya kuishi, ni mambo gani muhimu ya kuzingatia?
Vipengele vifuatavyo vitakusaidia kujua sera ya ufalme wa mbinguni, kuhusu ujenzi wa nyumba binafsi ya kuishi. Nia ya kukushirikisha vipengele hivi, ni ili kukupa mistari ya biblia, iwe msingi wa imani yako, wakati unapoamua kuwa na nyumba yako ya kuishi – iliyo mali yako!

Kipengele cha 1: Usijenge nyumba yako ya kuishi, au usinunue nyumba ya kuishi, bila kumshirikisha Mungu katika kila hatua. Hii ni kwa sababu biblia inasema: “Bwana asipoijenga nyumba, waijengao wafanya kazi bure” (Zaburi 127:1)

Kipengele cha 2: Pokea kama wazo la Mungu, ile hamu inayokuja moyoni mwako kukuhimiza ujenge nyumba (au ununue nyumba), ili iwe yako ya kuishi.Hivi ndivyo mfalme Sulemani alivyopokea msukumo wa kujenga nyumba ya Bwana, na nyumba yake mwenyewe!
Ripoti ya ujenzi wa nyumba zote hizo mbili inasema: “Hivyo Sulemani akaimaliza nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme; na yote yaliyomwingia Sulemani moyoni ayafanye nyumbani mwa Bwana, na nyumbani mwake mwenyewe, akayafanikisha” (2 Mambo ya Nyakati 7:11). Soma pia 2 Mambo ya Nyakati 8:1 na Mhubiri 2:4).

Kipengele cha 3: Ni sehemu ya mapenzi ya Mungu yaliyomo katika agano lake kwa ajili yako, ya kwamba uwe na nyumba ya kuishi, iliyo mali yako – tena iliyo nzuri – na uweze kuishi ndani yake (Kumbukumbu ya torati 8:12).

Kipengele cha 4: Moyoni mwako Mungu atakupa kujua mahali pa kujenga (au kununua) nyumba ya kuishi – palipo salama, na penye amani na utulivu. Hii ni kwa sababu Mungu anasema: “Na watu wangu watakaa katika kao la amani; na katika maskani zilizo salama, na katika mahali pa kupumzika penye utulivu” (Isaya 32:18).

Kipengele cha 5: Kiwanja unachotaka kukitumia kujenga nyumba yako ya kuishi, ni budi kiwekwe wakfu kwa maombi (kuombewa), kabla hujaanza kujenga.Haya ni maelekezo yaliyopo katika Isaya 45:1 – 4 ..kwa ajili ya eneo la kukaa/kuishi makuhani! Na kufuatana na Ufunuo wa Yohana 5:9,10, kila anayemjua Yesu kama Bwana na Mwokozi, amefanyika kuhani kwa Mungu, kwa damu ya Yesu Kristo
Nitaendeleza somo hili wiki ijayo. Ni maombi yangu kwa Mungu katika jina la Yesu, Mungu akuwezeshe kujenga nyumba ya kuishi – na uweze kuishi ndani yake!

Kipengele cha 6: Moyoni mwako – Mungu atakuwekea kujua aina ya nyumba ya kujenga ili uweze kuishi ndani yake.
Kumbukumbu ya torati 8:12 imeita aina ya nyumba hiyo kuwa ni “nyumba nzuri”. Biblia katika 2 Mambo ya Nyakati 7:11 inatueleza ya kuwa mfalme Sulemani alipewa maelekezo ya kujenga nyumba yake ya namna hii!
Familia ya mama wa Shunemu (2 Wafalme 4:8 – 17) ilijikuta imejenga nyumba yao ya kuishi, na kukaa ndani yake, lakini wakasahau kuweka chumba kingine muhimu!Chumba hicho ndicho kilichokuwa kimebeba mlango wa baraka yao ya kupata mtoto – maana walikuwa hawana mtoto.
Baadaye walijenga chumba hicho, na nabii Elisha akakaribishwa kulala kwenye chumba kile, na kupata “kibali” kwa Mungu cha kuwaombea ili wapate mtoto!
Usijenge nyumba kwa kuiga! Sikiliza maelekezo ya Mungu anayoweka moyoni mwako, kwa ajili ya aina ya nyumba anayotaka ujenge na uishi ndani yake. Kila chumba kina baraka yake! Soma Mithali 3:33 inasema; “…Bwana …huibariki maskani ya mwenye haki”.

Tena biblia inasema; “Nyumba hujengwa kwa hekima…na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa vitu vyote vya thamani na vya kupendeza” (Mithali 24:3,4). Na “nyumbani mwake mna utajiri na mali” (Zaburi 112:3).

Kipengele cha 7: Kabla ya kuanza kujenga, unatakiwa kuhesabu gharama!
Yesu Kristo alisema: “Maana ni nani katika ninyi kama akitaka kujenga mnara asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kama anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumalizia baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumalizia” (Luka 14:28 – 30).
Hata ujenzi wa nyumba ni vivyo hivyo! Unatakiwa uhesabu gharama za kujenga hiyo nyumba, kabla ya kuanza kujenga.
Jambo hili litakusaidia kutathmini juu ya imani yako katika kumshirikisha Mungu katika ujenzi huo!
Yesu alisema ya kuwa – Yeye ni “alfa na omega, mwanzo na mwisho” (Ufunuo wa Yohana 1:8). Kwa hiyo, Yesu ni mwanzilishi wa chochote kinachoanza katika imani yake, na pia ni mkamilishaji katika imani, chochote kilichoanza na kuendelea au kuendelezwa katika imani.

Sera hii ya ufalme wa mbinguni juu ya ujenzi wa nyumba ya kuishi, inadai ushiriki wa Mungu kuanzia katika wazo la kujenga hadi kuanza kujenga, na kuendelea kujenga, hadi kumaliza kujenga.

Kumbuka: Hata kama una fedha kidogo bado unaweza ukaanza kujenga kwa imani – huku ukiwa na uhakika moyoni mwako (Waebrania 11:1), ya kuwa Mungu atakuwezesha hatua kwa hatua hadi umalize kujenga hiyo nyumba (Wafilipi 4:19,13).
Mungu aendelee kukubariki unapoendelea kuyatafakari haya niliyokushirikisha!

Na Mwalimu  Christopher & Diana Mwakasege(Mana Ministry)