Sifa za ufalme wa Mbinguni

Ufalme wa Mbinguni siyo dini, Ufalme wa Mbinguni ni nchi, tunapata uthibitisho huu wa kwamba mbinguni ni nchi kutoka kwenye katiba yetu (Biblia) katika kitabu cha Waebrania 11:15-16  maneno ya Mungu yanasema hivi:- “15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16 Lakini badala yake wanatamani nchi iliyo bora zaidi, yaani, nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandalia mji kwa ajili yao” .

Yesu Kristo alipokuja duniani hakuleta dini, bali alileta kile ambacho Adam wa kwanza alikipoteza, ambacho ni ufalme. Kwa hiyo lengo la Yesu kuja duniani lilikuwa ni kuuleta tena ufalme wa Mbinguni duniani, na hii tunaipata kutoka Luka 4:43 “Lakini Yeye akawaambia, “Imenipasa kuhubiri Habari Njema za Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa maana kwa kusudi hili nilitumwa.”

Ufalme wa Mbinguni una sifa zifuatazo:-

 • Ufalme wa Mbinguni una mfalme.

Katika ufalme wa Mbinguni Yesu Kristo ndiye mfalme.  “Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka (ufalme) yote mbinguni na duniani” Mathayo 28:18.  “13 Nakuagiza mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai na mbele za Kristo Yesu ambaye alipokuwa anashuhudia mbele ya Pontio Pilato alikiri ukiri mzuri, 14 uishike amri hii bila dosari wala lawama mpaka kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, 15 ambaye Mungu atamleta kwa wakati wake mwenyewe, Yeye ahimidiwaye, aliye peke yake Mtawala, Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.”1Timotheo 6:13-15.

 • Ufalme wa Mbinguni una  eneo la kutawala (himaya).

Zaburi 47:2 “Kwa kuwa BWANA aliye juu, mwenye kuogofya, Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.”  zaburi 24:1 “Nchi ni mali ya BWANA pamoja na vyote vilivyomo ndani yake, Dunia nao wote wakaao ndani yake”.

 • Ufalme wa Mbinguni una  raia. 

Unapompoke Bwana Yesu kama Bwana na mwokozi, unapewa uraia wa Mbinguni, kwa hiyo sisi tunao uraia wa duniani na wa Mbinguni (Dual citizenship). Wafilipi 3:20 “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni: kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo.”  Yohana 17:14,16.

 • Ufalme wa Mbinguni una  katiba na sheria.

Katiba inatoa kanuni na taratibu ambazo raia wanazitumia ili waweze kuishi na kutawaliwa. Katika ufalme wa Mungu katiba inaitwa Biblia. Pia ujulikana kama neno la Mungu au sheria ya Mungu. Mathayo 5:18 “18Kwa maana,amin, nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yo yote kutoka kwenye Torati mpaka kila kitu kiwe kimetimia.”

 • Ufalme wa Mbinguni una  lugha ya taifa.

Kunena kwa lugha ndiyo lugha ya taifa katika ufalme wa Mungu, Matendo ya mitume 2:1-4 “Ilipowadia siku ya Pentekoste, walikuwa wote mahali pamoja. 2 Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo uliotoka mbinguni, ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. 3Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao. 4 Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia”.

 • Ufalme wa Mbinguni una  utamaduni (Tunda la Roho pamoja na kusifu na kuabudu).

Kusifu na kuabudu ni utamaduni katika ufalme wa Mbinguni ufunuo 4:8 “Kila mmoja wa hawa viumbe wenye uhai wanne, alikuwa na mabawa sita na kujawa na macho pande zote, hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawakuacha kusema: ‘‘Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako, aliyeko na atakayekuja.’’

Tunda la Roho pia ni utamaduni wa Mbinguni ambao ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi. Wagalatia 5:22-23

 • Ufalme wa Mbinguni una  serikali.

Kanisa siyo chombo cha kidini, bali kanisa ni muundo wa serikali iliyopewa mamlaka ambayo Mfalme (Yesu Kristo) hutumia ili kuutawala ufalme wake. Mathayo 16: 18-19 ‘‘Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, hata malango ya kuzimu hayataweza kulishinda. 19Nitakupa funguo za Ufalme wa Mbinguni na lo lote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, lo lote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.’’

 • Ufalme wa Mbinguni una jeshi.

Jeshi la Mbinguni ni malaika, raia walioko katika ufalme wa Mungu wanalindwa na malaika. Zaburi 34:7 “Malaika wa BWANA hufanya kituo akiwazunguka wale wamchao, naye huwaokoa.”

 • Ufalme wa Mbinguni una ulipaji wa kodi (fungu la kumi).

Sisi kama raia wa ufalme wa Mungu, tunatakiwa kulipa kodi(zaka / fungu la kumi). Malaki 3:8-10 “8 ‘‘Je, mwanadamu atamwibia Mungu? Hata hivyo mnaniibia. ‘‘Lakini mnauliza, ‘Tunakuibia kwa namna gani?’ ‘‘Mnaniibia zaka(mnaniibia kodi) na dhabihu. 9Mko chini ya laana, ninyi taifa lote, kwa sababu mnaniibia mimi. 10Leteni zaka kamili(leteni kodi kamili) ghalani , ili kiwemo chakula katika nyumba yangu. Nijaribuni katika hili,’’ asema BWANA Mwenye Nguvu, ‘‘nanyi mwone kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni na kuwamwagieni baraka nyingi mpaka mkose nafasi ya kutosha au la.”

 • Ufalme wa Mbinguni una Mabalozi.

Tumechaguliwa na Mungu na kuteuliwa kama mabalozi ili kuwakilisha matakwa na mawazo ya ufalme wa Mungu. Mkakati wa Mungu wa kueneza habari njema ya ufalme ulikuwa ni kutumia mabalozi. 2Korintho 5:20 “Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, kana kwamba Mungu anawasihi kwa kupitia vinywa vyetu, nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Kristo, mpatanishwe na Mungu.”

 • Ufalme wa Mbinguni una Mwanasheria mkuu ambaye  ni Roho mtakatifu.

Roho mtakatifu ni mwanasheria mkuu wa Mbinguni, yeye ndiye aliyehusika katika uandikaji wa katiba(Biblia) 2:Petro 1:20-21. Roho mtakatifu kama mwana sheria mkuu katika ufalme wa Mungu, yeye ndiye anayehusika katika kuwaongoza na kuwafundisha raia wa ufalme wa Mungu jinsi ya kusema wanapopelekwa mbele ya mabalaza na mahakama au masinagogi, unaposoma kitabu cha Luka 12:11-12  neno la Mungu linasema hivi:- ‘‘Watakapowapeleka katika masinagogi mbele ya watawala na wenye mamlaka, msiwe na wasiwasi kuhusu namna mtakavyojitetea au mtakavyosema: 12Kwa maana Roho Mtakatifu atawafundisha wakati uo huo mnachopaswa kusema.”

 • Ufalme wa Mbinguni una fedha(currency) ambayo ni imani.

Ufalme wa Mungu ni nchi ambayo fedha yake ni imani. Huwezi ukafanya biashara yoyote katatika ufalme wa Mungu bila ya kuwa na imani. Kama vile ambavyo huwezi kuishi katika nchi yoyote duniani bila fedha, vilevile huwezi kuishi katika ufalme wa Mungu bila ya kuwa na  imani (Warumi 1:17, Marko 5:34).

 • Ufalme wakili mkuu una wakili mkuu ambaye ni Yesu Kristo.

1Yohana 2:1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikieni haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu ye yote akitenda dhambi, tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo Mwenye haki.

 • Ufalme wa Mbinguni una hakimu mkuu (Mungu).

Na mbingu zitatangaza haki yake, kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu (Zaburi 50:6).

By
Dawson Kabyemela
Kingdom Influence Network.