KATIBA YA UFALME WA MUNGU

MAMBO 15 MUHIMU UNAYOPASWA KUJUA KUHUSU UFALME WA MUNGU.

JAMBO LA KWANZA : KATIBA YA UFALME WA MUNGU.

Tumezaliwa na kukulia kwenye jamii zenye mitazamo ya kidini, kwa hiyo imekuwa ni vigumu sana kuelewa na kufuata kanuni na taratibu za Ufalme wa Mungu ambazo zenyewe ziko tofauti kabisa na za dini, pia tunamwamini Yesu, tunamtumikia Yesu na kumfuata Yesu Kristo ambaye ni Mfalme kwa fikra na mitazamo ya kidini. Yesu hakuleta dini duniani bali alileta Ufalme. (Mathayo 4 : 17 ).

Kama tulivyoona kwenye utangulizi, Mbinguni ni nchi na ni nchi ya kifalme, katika utaratibu wa kawaida kabisa hakuna nchi yoyote au ufalme wowote unaoweza kuongozwa bila ya kuwa na katiba.

Katiba imebeba sheria, taratibu, kanuni, wajibu na miongozo ya aina mbali mbali ambayo inamwongoza raia jinsi ya kuishi katika nchi.

KATIKA UFALME WA MUNGU KATIBA NI BIBLIA, pia inajulikana kama neno la Mungu au sheria ya Mungu.

Watu wengi sana wameshindwa kuielewa Biblia, wengi wanaitafsiri Biblia kama kitabu cha dini ya kikristo. Ili uisome na uielewe biblia vizuri na kufahamu fikra na mawazo ya Mungu, unatakiwa kuisoma Biblia ukiwa na mtazamo ufuatao, kwanza tambua kwamba biblia ni kitabu kinachozungumzia mambo makuu matatu ambayo ni :-

  1. Mfalme (Serikali)
  2. Ufalme (Nchi)
  3. Familia ya mfalme (Raia)

ukiisoma Biblia ukiwa na mtazamo huu hapo ndipo utakapo ielewa, tofauti na hapo hutaelewa.

Katika ufalme wa Mungu Katiba ya nchi inatokana na mawazo / matakwa ya Mfalme (“BWANA alipomaliza kusema na Musa juu ya Mlima Sinai, Mungu akampa vibao viwili vya Ushuhuda, vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu.”kutoka 31:18)

Biblia ni katiba ya ufalme wa Mbinguni hapa duniani, na Biblia iliandikwa kwa nguvu za Roho mtakatifu (2Timotheo 3:16, 2Petro 1:21), Roho mtakatifu ambaye ni mwanasheria mkuu wa ufalme wa mbinguni. Biblia siyo kitabu cha dini ya Kikristo bali ni katiba kutoka Mbinguni ambayo imebeba sheria, kanuni, wajibu na miongozo ya aina mbali mbali ambayo inamwongoza mwanadamu jinsi ya kuishi katika ufalme wa Mungu.

Mungu alimwambia Yoshua hivi “Kitabu hiki cha Torati (BIBLIA) kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapoifanikisha njia yako na kisha utasitawi sana” Yoshua 1:8.

Kwa hiyo sisi kama raia wa mbinguni imetupasa kuisoma sana katiba (Biblia) na kuielewa kuliko kitabu kingine chochote duniani ili tupate kujua haki na wajibu wetu tulio nao katika Ufalme wa Mungu.(wafilipi 3:20).

Asante na Mungu akubariki sana.

© Mwalimu D. R. Kabyemela

© 0714 606500  /  0757 263 226

© Ufalme wa Mungu Kwanza

© www.kinet.org/umk

© info@kinet.org

© U M K

Leave a Reply