URAIA WA MBINGUNI

MAMBO 15 MUHIMU UNAYOPASWA KUJUA KUHUSU UFALME WA MUNGU.

JAMBO LA PILI : URAIA WA MBINGUNI.

Jambo la pili na la muhimu kujua kuhusu Ufalme wa Mungu ni URAIA WA MBINGUNI.

 

Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko MBINGUNI; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; (Wafilipi 3 : 20 )

But our CITIZENSHIP is in heaven. And we eagerly await a Savior from there, the Lord Jesus Christ. (Philippians 3 : 20  NIV )

Uraia ni hadhi anayokuwa nayo mtu, kwa kuzaliwa au kwa kupewa, ya kufaidika na kuwajibika kwa nchi fulani, kutokana na kuwa sehemu halali ya jamii ya nchi husika. Inajumuisha; haki ya kumiliki au kufaidika na raslimali za taifa, kupiga kura, kupata hati ya kusafiria nk ni hali ya kuwa raia wa nchi kama Tanzania. Kuwa raia kunakufanya kujiunga na eneo la kijiografia na kwa jamii ambayo inatawaliwa na sheria, ambapo kila mtu ana haki na wajibu.

Mwanadamu alipomwasi Mungu kati ya mambo muhimu sana aliyonyangaywa na Mungu ulikuwa ni URAIA WA MBINGUNI.

Mwanadamu alipoasi alinyanganywa passport ya Mbinguni akabaki duniani kama balozi bila hati, mwanadamu akawa mjumbe bila hadhi ya kiofisi, mwanadamu akawa raia bila nchi, mwanadamu akawa mfalme bila ufalme, mwanadamu akawa mtawala bila miliki, mwanadamu akawa mtoto bila Baba, mwanadamu akawa mkimbizi duniani.

ULIMWENGU WA MWILI NA ULIMWENGU WA ROHO

ULIMWENGU WA MWILI

Ulimwengu wa mwili ni ulimwengu wa damu na nyama yaani ulimwengu unaoonekana kwa macho ya kawaida. Na kila mwanadamu katika ulimwengu huu wa mwili ana uraia wake. Kwa mfano sisi ni raia wa Tanzania kwa sababu tumezaliwa Tanzania, na tuna haki zetu kama watanzania.

Sifa za uraia wa ulimwengu wa mwili:-

Uraia wa ulimwengu wa mwili una kikomo,

Uraia tulionao hivi sasa wanadamu ni uraia wa kupita tu.

Uraia usiokuwa na makazi ya kudumu,

Uraia usiokuwa na uzima wa milele ndani yake.

Uraia wenye kuharibika
Uraia huu kikomo chake ni pale mtu anapofariki.

Kifo maana yake ni utengano kati ya mwii na Roho.

Kuna aina tatu za kifo:-

1) Kutengana roho na mwili,

2) Kutokumwamini Yesu Kristo na kumpokea kwenye maisha kama Bwana na mwokozi wa maisha yako (Efeso 2:1, 6).

3) Kule kutupwa jehanamu ya moto.

ULIMWENGU WA ROHO

Mwanadamu ni roho inayoishi katika nyumba inayoitwa mwili, ana sehemu kuu tatu ambazo ni NAFSI, MWILI na ROHO. Ulimwengu wa roho ni mahali ambapo roho zinakaa. Huku ndipo ambapo nafsi na roho zetu zinakaa.
Katika ulimwengu wa roho kuna falme za aina mbili:

1) kuna Ufalme wa Mungu tunayemwabudu katika Kristo Yesu (Ufalme wa Mbinguni).

2) Ufalme wa shetani

Sasa nisikilize kwa makini;

Katika ulimwengu wa roho kila mwanadamu ni raia ama wa Ufalme wa Mungu au Ufalme wa shetani, hakuna mwanadamu ambaye hana uraia katika ulimwengu wa roho. Inawezekana unajua ama haujui lakini fahamu hivi kama haupo kwenye ufalme wa Mungu upo kwenye ufalme wa shetani.

Sifa za uraia wa ulimwengu wa roho:-

Uraia wa ulimwengu wa roho hauna kikomo ni wa milele.

Uraia ulio na makazi ya kudumu,

Uraia ulio na uzima wa milele ndani yake.

Uraia usio na mwisho

Tambua hili;

  • Makao makuu ya Mungu ni Mbinguni
  • Makao makuu ya wanadamu ni Duniani
  • Na makao makuu ya shetani ni Kuzimu

INSI YA KUPATA URAIA / WENYEJI WA MBINGUNI

Unapomkiri Yesu Kristo awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako maana yake unakuwa umezaliwa mara ya pili katika ulimwengu wa roho.  Na siyo kuzaliwa mara ya pili tu bali unapewa uraia wa Mbinguni. ( Warumi 10 : 9-10 ).

Mtu mmoja Mfarisayo jina lake Nikodemo mkuu wa Wayahudi huyu alimjia Yesu usiku na kumuuliza habari ya miujiza ambayo Yesu anaifanya, Yesu alimjibu hivi “amin, amin, nakuambia, mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona UFALME WA MUNGU ”. Nikodemo akaendelea kuuliza “mtu awezaje kuzaliwa mara ya pili akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?” Yesu akamjibu hivi:- ‘‘Amin, amin nakuambia, hakuna mtu ye yote anayeweza kuingia katika UFALME WA MUNGU isipokuwa amezaliwa kwa maji na kwa Roho. Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho. Kwa hiyo usishangae ninapokuambia huna budi ‘kuzaliwa mara ya pili’”. Yohana 3:1-7.

Unaposoma Wakolosai 1 : 13 anasema hivi “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;”

“…furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa MBINGUNI” (Luka 10:20).

Kwa hiyo tunapompokea Bwana Yesu tunaamishwa kutoka kwenye Ufalme wa shetani ( KUZIMU ) tunaingizwa kwenye UFALME WA MUNGU ( MBINGUNI )  na kupewa moja kwa moja uraia wa Mbinguni.

Wale wote ambao hawajampokea Bwana Yesu wapo kwenye ufalme wa Shetani katika ulimwengu wa roho hata wakifa wanaenda kuzimu moja kwa moja.

Haijalishi wewe ni mwimbaji mzuri wa kwaya au wewe ni mtoaji mzuri wa sadaka lakini kama haujazaliwa mara ya pili bado wewe ni RAIA WA KUZIMU. Yesu mwenyewe alisema mtu asipozaliwa mara ya pili hawezi kuuona ufalme wa Mbinguni.

Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.

Asante na Mungu akubariki sana.

© Mwalimu D. R. Kabyemela

© 0714 606 500 / 0757 263 226

© Ufalme wa Mungu Kwanza

© www.kinet.org/umk

© info@kinet.org

© U M K

Leave a Reply