MAMBO 15 MUHIMU UNAYOPASWA KUJUA KUHUSU UFALME WA MUNGU.

JAMBO LA SABA : JESHI LA UFALME WA MUNGU.

Zaburi 34:7

“MALAIKA wa BWANA hufanya kituo akiwazunguka wale wamchao, naye huwaokoa.”

Unapookoka unaingia kwenye UFALME WA MUNGU na huko unakutana na MAJESHI YA UFALME ambao ni MALAIKA WATAKATIFU.  MALAIKA ni POLISI WA UFALME na pia ni WANAJESHI WA UFALME lakini kama hujui kuwatumia wanakuwa hawafanyi kitu ndani ya Ufalme. Kuna mambo mengine ambayo sisi tunafanya kama WANA WA UFALME, kuna mambo mengine ambayo MALAIKA wanayafanya na kuna mambo mengine Neno la Mungu linayafanya na sio sisi. Kwa mfano:-

Luka 10:19 “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”

Maana yake ni sisi tunaokanyaga si Mungu, Unaweza kumkuta mtu anamwomba Mungu ashuke aje akibariki chakula chake na ashuke amlinde usiku kucha kitu ambacho hakiwezekani kwa Mungu kutoka kwenye kiti chake cha Enzi kwenda nyumbani kwa mtu kumlinda. hivyo ndivyo tulivyokuwa tukiamini lakini sasa tumeshafahamu maarifa kwamba siri ya Nguvu zetu Kuwa ndani ya UFALME WA MUNGU kuishika katiba yake ambayo ndiyo inatupa maelekezo ya namna ya kutenda hapa duniani.

JESHI LA UFALME WA MUNGU

Ndani ya UFALME WA MUNGU kuna MAJESHI, kuna nchi inaitwa MBINGUNI, ambayo sisi tuliookolewa tunaishi ndani yake katika ulimwengu wa roho. Yesu alisema mtu lazima azaliwe mara ya pili ndipo aingie kwenye UFALME WA MUNGU awe RAIA WA MBINGUNI. JESHI hili la Ufalme linaitwa MALAIKA WATAKATIFU. Malaika hawa ni watumishi wetu ambao wanatutumikia na kutulinda.

MALAIKA ni WANAJESHI wa Jeshi la UFALME WA MUNGU ambao kazi yao ni kuwatumikia RAIA WA UFALME WA MUNGU kwa kuwalinda wao pamoja na mali zao. Pia kuna kazi nyingine wanazofanya kulingana na sheria zinazoongoza majukumu yao katika ufalme.

Unapowatumia MALAIKA fahamu kwamba wana lugha zao ambazo ni BIBLIA (KATIBA) ambayo ni Neno la Mungu na KUNENA KWA LUGHA (LUGHA YA UFALME), unapomtuma malaika uwe unataja sheria inayomhusu kwenye Biblia na uombe.

Wewe kama RAIA WA UFALME WA MUNGU ni muhimu sana kujua jinsi ya kutumia JESHI LA MALAIKA, kujua umbo la Malaika, na jinsi ya kuwasiliana na Malaika maana sio mambo yote ni ya kuomba mengine ni ya kuamuru MALAIKA tu. Lakini kutokana na kutokujua wengi malaika wao wamekaa bila kufanya kazi.

Ili uweze kutumia malaika kwenye kila eneo la maisha yako ni vizuri kufahamu LUGHA YA MALAIKA, namna wanavyotenda kazi pamoja na siri nyingi zinazohusu malaika.

Biblia inasema Malaika alishuka toka mbinguni kwenye kaburi la Yesu ambapo wale walinzi walipomwona walizimia wakawa kama wafu, ndipo tunaanza kufahamu kwanini Malaika wawili peke yao waliichoma sodoma na gomora. Unapoomba saa nyingine haujibiwi sababu unaagiza Malaika elfu moja wakati Malaika mmoja anatosha kumpiga yule anayekusumbua.

MATHAYO 28: 1 “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu.”

MALAIKA NI ROHO watumikao katika UFALME WA MUNGU, kila mtu aliye ndani ya UFALME WA MUNGU anao Malaika wake wa kumtumikia. Unapokuwa kwenye UFALME WA MUNGU unatakiwa uwatumie Malaika na sio kuwaabudu unasema katika jina la Yesu namtuma Malaika aende afanye kitu fulani.

Matendo ya mitume 5: 19 “lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema,”

Huyu MALAIKA ameenda mpaka gerezani akawatoa watu wa Mungu gerezani. Tunajifunza wakati wa kwenye maombi unaweza kumtuma MALAIKA huyu aende akafungue milango ya biashara iliyofungwa, ndoa illiyofungwa, kazi, milango ya kupata kiwanja, milango ya kupata visa, milango ya promotion iliyofungwa na akaenda kufungua milango uliokwama kwa damu ya Yesu. Watu wa duniani kwenye Ufalme wao huenda kwa waganga wa kienyeji lakini sisi Mungu wa Ufalme wetu anazo nguvu nyingi kuliko mungu wao na tunaweza kutenda mambo makubwa kuliko wao.

 

Asante sana na Mungu akubariki.

© Mwalimu D. R. Kabyemela

© Ufalme wa Mungu Kwanza

© www.kinet.org/umk

© info@kinet.org

© U M K