Mathayo 6 : 31 – 33

MSISUMBUKE, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?
Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.

MSISUMBUKE – Do not Worry ( Msiwe na wasiwasi , Msihangaike, Msiwe na mashaka, Msiwe na dukuduku ).

Kati ya dhambi tunayoitenda kila siku mbele za Mungu ni kuwa na wasiwasi au mashaka kuhusu chakula, mavazi , ada za watoto , kodi za nyumba na vitu vingine kama hivyo, wakati Mungu anasema hivi vitu tusiviwaze wala kuvisumbukia. Dhambi ni kuambiwa usifanye kitu fulani halafu ukafanya.

Pamoja na kwamba kuwaza na kusumbukia hivi vitu ni dhambi, pia kiafya husababisha magonjwa kama Presha, msongo wa mawazo na vidonda vya tumbo, ndo maana Mungu anatusihi tusivisumbukie  hivi vitu.

Badala ya kusumbukia hivi vitu Mungu anataka nini kwako?, jibu ni hili hapa “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”

Badala ya kusumbukia mavazi, chakula , ada za shule , kodi na vitu vingine kama hivyo Mungu anasema tafuta kwanza Ufalme wake halafu hivyo vitu vitakuaja vyenyewe. Unapoutafuta Ufalme wa Mungu unageuka unakuwa kama sumaku unavuta vitu kuja kwako. Usipoutafuta ufalme wa Mungu wewe utakuwa ukifukuzana na vitu hivyo kila siku kuvitafuta.

Mtu anaweza akawa anajiuliza ni namna gani naweza kuutafuta Ufalme wa Mungu na haki yake, jibu ni rahisi sana nalo ni KUTAFUTA NA KUTAMBUA KUSUDI LA KUUMBWA KWAKO NA KUANZA KULIFANYIA KAZI, kwa sababu Mungu anakulisha na kukutunza kadri unavyolitumikia KUSUDI LA KUUMBWA KWAKO.

Daktari aliyeajiriwa na serikali hawezi kutunzwa na kulipwa mshahara asipotibu wagonjwa, kazi ya daktari ni kutoa tiba kwa wagonjwa. Daktari akitoka hospitali na kuacha wagonjwa wanakufa akaenda kufanya kazi ya uhasibu hawezi kulipwa na serikali.

MAMBO YATAKAYOKUSAIDIA KUGUNDUA KUSUDI LA MUNGU NDANI YAKO.

  1. Ni mambo gani ukiwa unafanya unajisikia furaha, uko tayari kufanya hata bila ya malipo / yale ambayo ni zaidi ya chakula kwako.
  2. Ni jambo gani linalokutia hasira unapoliona linatendeka / linaendelea.
  3. Ni mambo gani / jambo gani watu wanakuja kwako kuhitaji msaada mara kwa mara.
  4. Kitu gani unaweza kufanya kwa urahisi bila kutumia nguvu sana.
  5. Kitu gani ambacho ukikifanya kinakupa amani na kuufanya moyo wako ujisikie utoshelevu.
  6. Kitu gani unaweza kukifanya na kuleta faida kwako au kwa dunia yako.

UKISHUGHULIKA NA MAMBO YA MUNGU NA MUNGU ATASHUGHULIKA NA MAMBO YAKO, HIVYO KILA SIKU BADALA YA KUWAZA  NITAKULA NINI, NITAKUNYWA NINI AMA NITAVAA NINI WEWE WAZA NITAFANYA NINI KWA AJILI YA UFALME WA MUNGU.

Asante na Mungu akubariki sana.

© Mwalimu D. R. Kabyemela

© Ufalme wa Mungu Kwanza

© www.kinet.org/umk

© info@kinet.org

© U M K