VITA YA MANENO – Bishop Sylvester Gamanywa

“Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; nao waupendao watakula matunda yake.” (Mith.18:21)

Naomba kuwasilisha ujumbe maalum kuhusu matumizi ya vinywa vyetu kwa nia ya kujifunza faida na athari zake. Ni muhimu kutambua ya kwamba maneno yatokayo katika vinywa vyetu ya nguvu. Maneno mazuri yana “nguvu za uumbaji” na maneno mabaya ni kama “silaha za maangamizi”.

Maandiko tuliyosoma hapa juu yanatujulisha jinsi ambavyo, nguvu za ulimi zimebeba mauti na uzima. Hebu tujihoji kwa kifupi hapa. Hivi kweli maneno yanayotoka vinywani mwetu yanazalisha matunda gani? Je! tunatumia maneno ya ndimi zetu kujenga au kuangamiza wengine?

Maneno yatokayo vinywani mwetu ni ya namna gani? Yamejaa sumu ya chuki au ladha ya upendo? Yamejaa sumu ya uchungu au dawa ya baraka? Ni maneno ya lawama au kutia moyo? Ni maneno yanayotabiri ushindi au kushindwa?

Maneno ni kama vifaa vya matumizi ya kutusaidia kufikia malengo ya kimaendeleo au kushusha moyo na kusababisha mkandamizo wa moyo na msongo wa mawazo.

WEMA NA UBAYA WETU HUJULIKANA KWA MANENO YETU

Kwa mujibu wa maneno ya Yesu, maneno ya vinywa vyetu ni akiba mbovu iliyomo katika mioyo yetu.

“Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya.” (Matt.12:34-35)

Kifungu hiki kinatujulisha jinsi ambavyo ubaya wa mtu unathibitishwa na maneno ya kinywa chake. Huwezi kujitangaza kuwa mwema wakati kinywa chako kinatema sumu yenye kunajisi na kuharibu maisha ya wengine. Na mtu mwema hata kama sura yake sio ya kuvutia, lakini kwa maneno mema ya kinywa chake huutambulisha uzuri na wema wake.

Kiashiria cha mabadiliko ya kitabia kwa mtu aliyekutana na nguvu za wokovu wa Yesu Kristo, ni maneno yatokayo katika kinywa chake. Haiwezekani mtu mwenye kutangaza hadharani kuwa “ameokoka” au “amezaliwa upya” halafu bado akabaki na kinywa chenye kutema maneno yenye sumu iliyooza kama mpagani asiyemjua Mungu hata kidogo! Yesu anasema mtu wa jinsi hii bado ni wa “uzao wa nyoka”!

Kwa uzoefu wangu katika huduma za kiroho, dalili mojawapo ya mtu aliyejawa na pepo wachafu ni maneno yanayotoka kinywani mwake. Kumbuka ya kwamba, pepo wachafu ndio chimbuko la maneno machafu pia.

Ukijikuta kila mara unatokwa na maneno machafu hata kama hupendi kuyasema lakini yanakutoka tu bila kujizuia, hizo ni dalili za pepo wachafu ndani yako, na njia pekee ni maombezi ya kufunguliwa kwa pepo hao kukemewa kwa mamlaka ya jina la Yesu yatoke upate kuwa huru! Ubishi na kujihami kwingi kwa visingizo vya madai ya ujasiri wa kuonya na kukemea wengine sio leseni ya kutokwa na maneno machafu yaliyooza! “Two wrongs does not make one right”

MANENO YETU YANA ASILI YA UMILELE

Maneno yetu sio kwamba yana nguvu za kusababisha mauti au uzima katika dunia hii, bali hata katika ulimwengu ujao ambao ni wa milele.

“Basi, nawambia, kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.” (Matt.12:36-37)

Hivi ndivyo maneno tusemayo kila siku yalivyo na nguvu za umilele. Tutakutana nayo siku ya hukumu. Na hakuna hata mmoja wetu ambaye hatakutana na Mungu siku ya hukumu. Kiburi chetu ni kifupi mno huwa kinayeyuka ghafla tunapofikwa na mauti. Na hata wengine wanaodai hawaogopi kifo mawazo yao hubadilika ghafla pale kifo kinapowafika na wakati huo tayari wamechelewa kwani huwa hawaweze kubadilisha kitu.

MAONYO KUHUSU KINYWA CHA MCHAJI MUNGU

“Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.” (Efe.4:29)
Kifungu hiki hapa juu Paulo anachambua kuhusu “wema dhidi ya uovu” kuhusu “maneno chanya” dhidi ya “maneno hasi” Msamiati wa kiyunani uliotumika wa neno “ovu” maana yake ni “uozo”! Lilitumika kutaja matunda au mboga zilizooza. Hali kadhalika, kuna maneno mengi “yaliyooza” yakitoka vinywani “yananuka” uchafu na kunajisi masikio na mioyo ya watu. Maneno ya jinsi hii hayapaswi kutoka kwenye kinywa cha mwenye kujitambulisha kuwa mtu wa Mungu, au mchaji Mungu.

Msisitizo wa Paulo kwa wacha Mungu ni kutumia vinywa vyetu kuachilia maneno yenye msaada wa kuwajenga wahitaji. Katika ulimwengu huu mahitaji siyo fedha au mali au vitu peke yake, bali hata “maneno yenye kujenga” ni bidhaa adimu katika jamii ya leo. Haya maneno mazuri ya kuwafaa wengine yametajwa tena katika waraka kama ifuatavyo:

“Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua iwapasavyo kumjibu kila mtu.” (Kol.4:6)

“Let your speech at all times be gracious and pleasant, seasoned with salt, so that you will know how to answer each one [who questions you].”

Kwa maandiko haya tunahimizwa kutumia vinywa vyetu kuwabariki wengine na sio kuwalaani na kuwabomoa. Maneno yetu yanatakiwa kuwa ya kuokoa na sio kuhukumu.

Mpendwa msomaji wa ujumbe huu. Ni wakati wa kujirudi na kujitakasa kwa maneno yasiyofaa yatokayo katika vinywa vyetu. Aidha, tujue ya kwamba maneno chanya na mema ni bidhaa adimu kwa kizazi chetu hiki. Ni wakati wa kutumika kuokoa, kufariji, kujenga, na kubariki. Kama ujumbe huu umekugusa nijulishe kwa ku-like post hii na ikiwezekana warushie na marafiki zako. Mimi nimetimiza wajibu wangu, na wewe pia timiza wajibu wako. Ubarikiwe sana!