Wazo kuu la Mungu

Watu wengi sana wameshindwa kuielewa Biblia, wengi wanaitafsiri Biblia kama kitabu cha dini ya kikristo. Ili uisome na uielewe biblia vizuri na kufahamu fikra na mawazo ya Mungu,  unatakiwa kuisoma Biblia ukiwa na mtazamo ufuatao, kwanza tambua kwamba biblia ni kitabu kinachozungumzia mambo makuu matatu ambayo ni :-
Mfalme (Serikali)
Ufalme (Nchi)
Familia ya mfalme (Raia)

ukiisoma Biblia ukiwa na mtazamo huu hapo ndipo utakapo ielewa, tofauti na hapo hutaelewa.
Biblia ni katiba ya ufalme wa Mbinguni hapa duniani, na Biblia iliandikwa kwa nguvu za Roho mtakatifu (2Timotheo 3:16, 2Petro 1:21), Roho mtakatifu ambaye ni mwanasheria mkuu wa ufalme wa mbinguni. Biblia siyo kitabu cha dini ya Kikristo bali ni katiba kutoka Mbinguni ambayo imebeba sheria, kanuni, wajibu na miongozo ya aina mbali mbali ambayo inamwongoza mwanadamu jinsi ya kuishi katika ufalme wa Mungu, Mungu alimwambia Yoshua hivi “Kitabu hiki cha Torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapoifanikisha njia yako na kisha utasitawi sana” Yoshua 1:8.

Kumbuka Mbinguni ni nchi na utawala wake ni wa kifalme, na katika kitabu cha Waebrania 11:15-16  maneno ya Mungu yanasema hivi “15 Kwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16 Lakini badala yake wanatamani nchi iliyo bora zaidi, yaani, nchi ya mbinguni”.

Hakuna ufalme wowote ambao unaweza kuongozwa bila kuwa na katiba, kwa hiyo sisi kama raia wa mbinguni imetupasa kuisoma katiba(Biblia) hii na kuielewa kuliko kitabu kingine chochote duniani ili tupate kujua haki na wajibu wetu tulio nao katika Ufalme wa Mungu.(wafilipi 3:20).

Wazo kuu la Mungu kuiumba dunia na kumweka mwanadamu lilikuwa ni:-

 •      Kupanua ufalme wake wa Mbinguni hadi duniani.
 •      Kuanzisha serikali ya ufalme wa Mbinguni duniani.
 •      Kuifanya dunia iwe koloni la Mbinguni (Mathayo 6:9-10).
 •      Kuijaza dunia utukufu, asili na utamaduni wa Mbingini. (Isaya 6:3, 11:9, Hesabu 14:21)
 •      Yeye Mungu kendelea kutawala Mbinguni halafu watoto wake wa kike na wa kiume watawale duniani kama makuhani na wafalme.(zaburi 115:16, Ufunuo 5:9-10, 1:6, Kutoka 19:6).
 •      Kusudi na mpango wa Mungu kuiumba dunia na kumweka mwanadamu lilikuwa ni kuongeza Ufalme wake wa Mbinguni hadi duniani na kushiriki utawala wake wa kifalme pamoja na watoto wake.

Mungu alitamani kuwa na familia ya watoto wa kiume na wa kike ambao wameumbwa kwa mfano wake na kwa sura yake ili kukamilisha mpango wake wa kuongeza ufalme wake wa Mbinguni hadi duniani. Na kazi ambayo alimpa mwanadamu ilikuwa ni kutawala dunia kwa niaba ya Mungu, ambayo inamaanisha mwanadamu alipewa uendeshaji, uongozi, usimamizi, madaraka, utumishi kwa niaba ya Mungu.

Kumbuka mwanadamu alipewa (stewardship) uendeshaji, usimamizi, uongozi na mamlaka ya kutawala na siyo umiliki, kwa sababu dunia na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana. Zaburi 24:1, Mwanzo 1:26 , zaburi 8:4-6, Isaya 45:11.

Mkakati wa Mungu ulikuwa ni kuwajaza Roho mtakatifu watoto wake wa kike na wa kiume ili kwamba wototo hawa waunganishwe na Mungu Baba wa mbinguni kwa njia ya Roho Mtakatifu mda wote wawapo duniani ili ufalme wa Mungu uje duniani na mapenzi yake yatimizwe huku duniani kama yanavyo timizwa huko Mbinguni, kwa maana hii huwezi kutimiza mapenzi ya Mungu duniani bila ya kuwa na ujazo wa Roho Mtakatifu.

ASILI YA DHAMBI/UASI NA MATOKEO YAKE. (Yatambue madhara ya dhambi)

Katika uumbaji, Mungu alimpa mwanadamu mamlaka ya kutawala vitu vyote alivyoviumba duniani, kwa hiyo mwanadamu alipewa usimamizi wa kazi ya Mungu kwa makubaliano  / mkataba / kwa masharti yafuatayo:- Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.(Mwanzo 2:16-17).

Maana yake Mungu alikuwa akimwambia mwanadamu kwamba, pamoja na kukupa mamlaka ya kutawala dunia, ila ni kwa mkataba kwamba /makubaliano maalum ambayo ni:-, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile. Na akasema hivi ukila adhabu yake ni kifo (Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti….. Warumi 6:23).

Maana ya neno kifo ni kutengwa na Mungu au kutoka katika uwepo wa Mungu.

Kumbuka Adamu alipokuwa akisaini mkataba huu wa utawala alikuwa akisaini kwa niaba ya wanadamu wote watakao zaliwa, hivyo kwa uasi wake huo ikawa ni kosa la kila mwanadamu ( warumi 5: 12, 17, 19)

Kwa hiyo kitendo cha Adamu kutii maneno yaliyotoka kwa shetani na kukubali kula tunda matokeo yake yalikuwa ni:-

 1. Adamu alikuwa anavunja mkataba na Mungu ambao malipo yake ni kifo (kutengwa na Mungu).
 2. Adamu alikuwa anatangaza uhuru wa dunia hii na kuiasi serikali ya mbinguni.
 3. Adamu alikabidhi tawala na miliki zote za dunia kwa adui shetani (Luka 4:5-7.
 4. Adamu alikuwa anaisaliti nchi/serikali yake ya Mbingini (uhaini).

Uharifu mkubwa sana ambao unaweza kufanywa dhidi ya serikali yoyote duniani ni uhaini, uhaini ni kitendo cha kuisaliti nchi au serikali yako. Uhaini ni kosa pekee ambalo ukilifanya huwezi kuepuka hukumu ya kifo au adhabu kali sana. Kitendo cha Adam kumwasi Mungu na kumtii shetani na kuamua kula tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya lilikuwa ni kosa la uhaini.

MATOKEO YA KUASI KWA MWANADAMU.

Kitendo cha mwanadamu kumwasi Mungu, alipoteza serikali pamoja na mifumo yote ya Ufalme wa Mungu, na hapo mwanadamu akaanzisha mifumo yake mwenyewe kama vile: mifumo ya Siasa, Uchumi, Elimu na mifumo ya kumtafuta Mungu na hapo ndipo tunapoanza kupata neno dini (Dini ni mfumo wa imani ambao umewekwa na kikundi cha watu fulani kwa ajili ya kumtafuta mungu wao).

Baada ya kuasi kwa mwanadamu alipoteza yafuatayo:-

 1. Alipoteza ufalme wa Mungu. Ndio maana imeandikwa utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake…………..(Mathayo 6:33).
 2. Alipoteza haki mbele za Mungu.
 3. Alipoteza lugha ya Mbinguni.
 4. Alipoteza utamaduni wa Mbinguni.
 5. Alipoteza maadili ya Mbinguni .
 6. Alipoteza uhuru wa kula matunda ya kila mti (free access).
 7. Alipoteza sheria za Mbinguni.
 8. Alipoteza mahusiano kati yetu na Mungu Baba yetu.
 9. Alipoteza desturi za Mbinguni.

10. Alipoteza mila za Mbinguni.

11. Alipoteza mifumo ya Mbinguni, mfano mfumo wa elimu, mfumo wa siasa, mfumo wa uchumi na mfumo wa biashara.

12. Alipoteza katiba ya Mbinguni.

13. Alipoteza mamlaka aliyopewa ya kuitawala dunia.

14. Alipoteza maisha (kifo).

15. Alimpoteza Roho mtakatifu.

16. Alipoteza nafasi ya ubalozi.

17. Alipoteza uraia wa Mbinguni.

18. Alipoteza Tunda la Roho (Upendo,Furaha, Amani, Uvumilivu, Utuwema, Fadhili, Uaminifu,Upole, Kiasi,

NB: ukitaka kujua zaidi kuhusu mwanadamu alichopoteza, fuatilia alicholeta Yesu, maana Yesu Kristo     alikuja kurudisha kile alichopoteza Adamu.

Baada ya uasi, mwanadamu akawa balozi bila hati, mwanadamu akawa mjumbe bila hadhi ya kiofisi, mwanadamu akawa raia bila nchi, mwanadamu akawa mfalme bila ufalme, mwanadamu akawa mtawala bila miliki, mwanadamu akawa mtoto bila Baba, mwanadamu akawa mkimbizi duniani.

By
Dawson Kabyemela,
Kingdom Influence Network.